Mwanariadha wa Afrika Kusini anayekabiliwa na kesi ya
mauaji, Oscar Pistorius, amedaiwa kuhusika katika malumbano ndani ya
klabu moja nyakati za usiku mwishoni mwa wiki.
Mwanariadha huyo alikuwa katika klabu moja
alipojikuta katika hali ya majibizano makali na mfanyabiashara mmoja
aliyekuwa amemuuliza kuhusu kesi anayokabiliwa nayo.
Mfanyabiashara huyo Jared Mortimer anayedaiwa kumshambulia Oscar kwa
maneno akimuuliza kuhusu kesi yake, anasema kuwa Pistorius alikuwa mlevi
chakari wakati wa majibizano hayo.
Sarakasi hiyo ilitokea katika klabu ya kifahari
mjini Sandton kufuatia madai kuwa Pistorius aliwatusi marafiki wa Jared
Mortimer pamoja na kuitusi familia ya Rais wa Afrika Kusini Jaocb Zuma.
Madai haya ni kwa mujibu wa jarida la The Star.
"Nilichukizwa sana na matusi aliyoyatoa
Pistorius kwa sababu nina uhusiano wa karibu sana na familia ya Zuma, ''
alisema bwana Mortimer.
Bwana Mortimer aliongeza kuwa mwanariadha huyo
alikuwa mlevi chakari na alianza kumsota kidole kifuani wakati
walipokuwa wakiongea.
Mfanyabaishara huyo alisema alimsukuma mwanariadha huyo ambaye alianguka chini.
Walinzi katika klabu hiyo, walimsaidia Pistorius
kusimama ingawa waliamrishwa kumpeleka nje ya klabu baada ya kuanza
kumtusi mwanamume mwingine.
Msemaji wa familia ya Pistorius Anneliese Burgess, amekanusha madai ya Mortimer.
Pistorius anakabiliwa na kesi ya mauaji ya
mpenzi wake Reeva Steenkamp yaliyotokea mwaka jana akisema kuwa alimuua
kwa bahati mbaya akidhani alikuwa jambazi aliyekuwa amevamia nyumba yao.
Kesi dhidi ya Pistorius iliahiirishwa wiki jana
tayari kwa kauli ya mwisho kutoka kwa upande wa utetezi na wa mashitaka
kabla ya uamuzi kutolewa.BBC
No comments:
Post a Comment