Watu watatu wa familia moja, akiwemo mwanafunzi wa sekondari,
wameuawa kinyama kwa kukatwa mapanga shingoni na sehemu mbalimbali za
miili yao na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema tukio hilo
limetokea juzi saa 2:30 usiku katika Kijiji cha Msungua, Kata ya
Irisya, Tarafa ya Sepuka wilayani Ikungi wakati wanafamilia hao wakiwa
wamelala ndani.
Alisema kuwa marehemu hao waligundulika baada ya majirani kuona mwili
wa mwanamke ukiwa nje, ndipo walianza kutaharuki na walipofuatilia
ndani walikuta mwili wa mwanaume ukiwa umelezwa kitandani.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Mussa Mkuki (92), mkewe Tatu Sefu (69)
na mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Gumanga wilayani Mkalama, Jasmin
Idd (17) ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika
zahanati ya Kijiji cha Sepuka.
Kamanda Kamwela alisema kuwa pia mwanafunzi wa darasa la tatu katika
Shule ya Msingi Kisuluda, Mussa
Nasoro, alijeruhiwa vibaya na kulazwa
katika hospitali ya Mkoa wa Singida huku hali yake ikielezwa kuwa
mbaya.
Uchunguzi wa daktari umebaini kuwa watu hao walipoteza maisha kutokana na kuvuja damu nyingi katika majeraha waliyoyapata.
Hadi sasa chanzo cha tukio hilo la kutisha hakijafahamika na Jeshi la
Polisi linaendelea na uchunguzi wake wa kina ili kubaini waliohusika.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment