Mfanyabiashara wa madini, Richard Lucas (29), amejipiga risasi
kichwani baada ya kusababisha ajali mbili tofauti na gari lake
kupinduka.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12 jioni nyumbani kwa marehemu eneo la Kimandolu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema kuwa Lucas alijipiga risasi ya kichwa kwa kutumia bastola aina ya Luger yenye namba B136986 baada ya kuwagonga watu hao.
Kamanda Sabas, alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini
kuwa Lucas alitokea Tengeru akiwa na gari aina ya Toyota Rav 4 yenye
namba za usajili T 494 CKY alikokuwa amemfuata rafiki yake aliyekuwa
amepata ajali ya kugongwa na gari.
Alisema kuwa walipofika eneo la Sekei Darajani, alimgonga mwendesha
pikipiki na kuendelea na safari ambapo mbele kidogo aligonga daladala
lenye namba za usajili T 636 CUR aina ya Nissan iliyokuwa inapakia
abiria.
Kamanda Sabas, alisema baada ya hapo gari ya Lucas ilipinduka na
waliokolewa kwa kupitia dirishani na wananchi, ndipo marehemu aliondoka
eneo la tukio kwa pikipiki ya kukodi akielekea nyumbani kwao Kimandolu
huku akimuacha Vick Mchuma kwenye eneo la tukio.
Alisema kuwa baada ya muda, Mchuma ambaye waliongozana naye kwenda
kumsaidia rafiki yao aliyepata ajali Tengeru, alipata taarifa kuwa Lucas
amejipiga risasi.
Katika tukio jingine, mpanda milima, Denis Joel, ameuawa kwa kuchomwa
na kitu chenye ncha kali chini ya bega la kulia karibu na moyo
alipotofautiana na mtu aliyekuwa akimdai shilingi 40,000.
Kamanda Sabas, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili
asubuhi kwenye Kitongoji cha Olturei-Moivo wilayani Arumeru.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Joel
alichomwa na kitu hicho na mtuhumiwa, Solomon Lembris, ambaye
walitofautiana kauli wakati wakidaiana fedha.
“Baada ya kuona jeraha, Joel aliamua kukimbia na Lembris aliendelea
kumkimbiza kuhitaji amlipe pesa zake ambapo aliishiwa nguvu na kuanguka
chini kisha kupoteza fahamu na kufariki dunia,” alisema Kamanda Sabas.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo, Lembris alitokomea kusikojulikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Tukio jingine ni la mkazi wa Sokon II, Arumeru, Lalaito Ngitoo (50),
aliyekutwa amekufa na mwili wake ukiwa kwenye maji ndani ya Mto Kijenge
bila jeraha.
Kamanda Sabas alisema tukio la kifo cha Ngitoo, lilitokea juzi majira
ya saa 11 ambapo kabla ya mwili wake kukutwa Mto Kijenge, alitoweka
nyumbani tangu Juni 7, mwaka huu.
Alisema kuwa Ngitoo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa ambao humsababisha kuanguka mara kwa mara.
Kamanda Sabas alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru.TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment