Polisi nchini Tanzania wamewakamata waganga wawili wa
kienyeji baada ya mwanamke mmoja mwenye ulemavu wa ngozi au Abino
kuuwawa kwa kuchinjwa.
Moja ya miguu yake pamoja na vidole
vilinyofolewa baada ya shambulizi hilo la hapo jana Jumanne katika mkoa
wa Simiyu Kaskazini Mashariki mwa Tanzania. Kumekuwa na visa vingi vya
mauaji ya albino katika eneo hilo hapo awali.
Shirika la kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi Albino la
'Under the Same Su'n limeiomba serikali ya nchi hiyo kufuta vibali na
shughuli zote za waganga wa jadi kwa madai kuwa wao ndiyo chanzo cha
kuuawa kwao.
Kuuawa kwa mwanamke Munghu Lugata mlemavu wa
ngozi toka kijiji cha Gasuma mkoani Simiyu Kaskazini Magharibi mwa nchi
hiyo kumeacha hisia na uchungu kwa walemavu wengine waliopata mikasa
hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa BBC Leonrad Mubali
kwa uchungu na kilio, Mariamu Staford mlemavu wa ngozi Albino amesema
kwamba tukio la kuuawa kwa Munghu Lugata mwanamke mwenye umri wa miaka
40 juzi linamkumbusha mkasa wake uliomkuta wa kukatwa mikono yake yote,
zaidi ya miaka mitano iliyopita na sasa anatumia mikono ya bandia ya
vyuma huku akisema malengo yake mengi yamekwama.
Albino wamekuwa wakihangaishwa sana nchini
Tanzania ambako baadhi ya watu wanaamini kuwa dawa za miujiza
zinazotengezwa kutokana na viungo vya miili yao zinaleta bahati nzuri.
Mashambulizi yamepungua katika siku za hivi
karibuni lakini mauaji ya hivi punde yamepelekea shirika moja la kutetea
haki za Albino kutoa wito kwa serikali kupiga marufuku waganga wote wa
kienyeji.
Matukio mengi ya maujia ya walemavu nchini
Tanzania yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina huku waganga wa
jadi wakihusishwa.
Mkoa wa Simiyu ni moja katika maeneo kaskazini magharibi mwa Tanzania yenye matukio mengi ya mauaji hayo.
Hivi karibuni nchini Tanzania umezinduliwa mnara
maalumu unaoitwa NITHAMINI, mnara pekee duniani unaowakilisha kupinga
mauaji ya albino huku Tanzania ikiwa ni moja ya nchi yenye matukio mengi
ya ukatili dhidi ya walemavu hao.BBC
No comments:
Post a Comment