Pages

Thursday, May 01, 2014

UBABE WATAWALA MALIASILI NA UTALII "WALIOFUKUZWA NA WAZIRI NYALANDU WARUDISHWA KAZINI"

Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama ubabe wa madaraka na kutoelewana ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Katibu Mkuu, Maimuna Tarishi, amepindua maamuzi ya Waziri wake, Lazaro Nyalandu na kuwarejesha kazini vigogo wa Wanyamapori waliokuwa wameng’olewa na waziri huyo.


Hivi karibuni Waziri Nyalandu aliwang’oa Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Sorongwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Bunge la Desemba 22, mwaka jana.

Azimio hilo lilifikiwa baada ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuonyesha kuwa watendaji wa Maliasili wakiwemo vigogo hao walizembea hadi wananchi wakatendewa unyama na wengine kupoteza maisha na mali zao.

Kwa hiyo Bunge liliitaka serikali iwawajibishe watendaji wote waliozembea akiwemo Profesa Sorongwa, ambaye alielezwa kuwa alitoa taarifa zisizo sahihi juu ya kuteswa kwa baadhi ya raia hao wema.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu Maimuna Tarishi ametengua uamuzi wa waziri wake na kuwarejesha vigogo hao kazini ili kuendelea na madaraka yao kama kawaida.

No comments:

Post a Comment