Pages

Thursday, May 22, 2014

MTOTO AFICHWA KWENYE BOKSI MIAKA MINNE


Mwanamke aliyetambuliwa kuwa ni Mariamu Said mkazi wa Kiwanja cha Ndege, Morogoro juzi alishushiwa kipigo na wananchi kutokana na kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne.


Tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi baada ya majirani zake kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.

Zongo alisema majirani hao walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa nje.

Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu Mgagala na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo na kumhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa akijibu kwa kubabaika.

Moja ya maswali aliyoulizwa ni idadi ya watoto wake na akajibu kuwa ana wawili lakini wakati akiendelea kujibu maswali, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na kumkuta mtoto Nasra akiwa ndani ya boksi.

Ofisa mtendaji huyo alisema wakati wakimtoa mtoto huyo ndani ya nyumba, kundi kubwa la watu waliokuwa na fimbo na mawe walianza kumshambulia mwanamke huyo na kumlazimu mtendaji kutoa taarifa polisi.

Alisema muda mfupi baadaye, polisi waliwasili na kumkamata Mariam na kumpeleka katika ofisi ya kata ambako aliwekwa chini ya ulinzi.

Baadaye aliwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa Jamii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema wanaendelea kukusanya taarifa za tukio hilo ikiwamo matokeo ya vipimo vya madaktari kuhusu afya ya mtoto huyo kabla ya kuchukua hatua zaidi.
Kamanda Paulo alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa kosa la kumfanyiwa mtoto vitendo vya kikatili.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema polisi wanakadiria kwamba mtoto huyo alianza kufichwa kwenye boksi hilo akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment