Maadhimisho ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo
kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana,
yameingia dosari baada ya ofisa wa Ikulu, Rashid John Chilwangwe
kufariki dunia akiwa katika maadhimisho hayo.
Chilwangwe alipatwa na tukio hilo majira ya saa nne asubuhi, nje ya
Uwanja wa Uhuru akiwa anasubiri kuingia na maandamano yaliyokuwa
yakipita uwanjani mbele ya Rais Jakaya Kikwete, yakitokea viwanja vya
Mnazi Mmoja.
Walioshuhudia tukio hilo, waliliambia gazeti hili kuwa Chilwangwe
ambaye anafanya kazi katika moja ya idara za Ikulu jijini Dar es Salaam,
alianguka ghafla na kisha kubebwa na wafanyafakazi wa Chama cha Msalaba
Mwekundu na kuhifadhiwa kwenye moja ya mahema yaliyoandaliwa uwanjani
hapo kwa ajli ya huduma za dharura.
Akiwa ndani ya hema hilo, baadhi ya madaktari walijitahidi kutoa
huduma ya kwanza ya matibabu, lakini hata hivyo wakati akiendelea kupata
matibabu alifariki dunia.
Haikuweza kujulikana sababu hasa ya kifo cha ofisa huyo wa Ikulu
kwani madaktari waliokuwapo eneo hilo hawakuwa tayari kuzungumzia kwa
kina tukio hilo la kusikitisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Englibert Kiondo, alikiri
kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema limetokana na Chilwangwe
kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kisukari.
Kiondo alisema kuwa kifo hicho kilichangiwa na mwendo mrefu
aliotembea na kusababisha kuamsha maradhi yake ya moyo na kisukari, na
hivyo kupoteza nguvu na kuanguka ghafla hatimaye kupoteza maisha.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment