Pages

Tuesday, May 06, 2014

GIGGS HATIHATI MAN UNITED



Kocha wa muda wa Manchester United, Ryan Giggs amesema ataacha kuifundisha Manchester United kwa ajili ya kwenda kupata zaidi mafunzo ya ukocha.
Giggs (40) hivi sasa ni kocha wa muda wa klabu hiyo baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa Manchester United, David Moyes kutimuliwa kutokana na timu kupata matokeo mabovu.

Tangu aanze kuinoa Manchester United, Giggs ameisimamia katika mechi mbili,  akiiongoza kushinda kwa mabao 4-0 katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Norwich City kabla ya kufungwa bao 1-0 na Sunderland Jumamosi iliyopita.

Leo, Giggs anatarajiwa kukiongoza kikosi cha Manchester United kupambana na Hull City katika mechi nyingine ya Ligi Kuu ya England ambayo inaelekea ukingoni.
Habari zilizopo ni kwamba baada ya msimu huu kumalizika, kocha Mholanzi Louis van Gaal ndiye atakayechukua jukumu la kuinoa Manchester United, ingawa zipo taarifa kwamba ataendelea kumtumia Giggs kama msaidizi wake.

Hata hivyo, juzi Giggs alitoa kauli ambayo inaonyesha anaweza kuondoka na kwenda klabu nyingine kwa ajili ya kufundisha soka.

“Ninaweza kuichezea Manchester United, siyo kwa sababu ya fedha kwani tayari nimepata mafanikio makubwa kwa kuichezea. Lakini mimi bado kijana katika suala la ukocha. Katika soka bado nina miaka 20 mpaka 25 kwa hiyo siyo lazima miaka hiyo niimalizie kwa kufundisha soka Manchester United, ninaweza kwenda klabu nyingine na kufundisha,”alisema Giggs.MWANANCHI


No comments:

Post a Comment