Pages

Friday, April 25, 2014

WANAUME CHANZO SARATANI MLANGO WA UZAZI KWA WANAWAKE


Wanaume wametajwa kuwa chanzo kikuu cha wanawake kupata ugonjwa wa saratani ya mlango wa uzazi ambayo imekuwa tishio kwa sasa.


Mshauri wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la PSI-Tanzania, Dk. Mashafi Joseph, alieleza hayo jijini Dar es Salaam juzi alipozungumza na waandishi wa habari, akizungumzia udhamini wao katika Jukwaa la Wanawake la ‘Familia kitchen party Gala’, litakalofanyika Aprili 27, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kupitia chapa yao ya familia.

Akifafanua hilo, Dk. Mashafi alisema kisayansi wanaume ndio wabebaji wa kirusi kinachosababisha ugonjwa huo kinachoitwa Human Papillomavirus (HPV) ambacho kwao hakina madhara ila kinapofika kwa mwanamke ndipo anapata saratani hiyo ambayo huambukizwa kwa njia ya kujamiana.

Kwa hapa nchini, alisema saratani hiyo sio tu inaongoza kwa vifo vya kinamama bali pia ni aina ya saratani ambayo inakua kwa kasi katika nchi za Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiwa na mzigo mkubwa wa wagonjwa.

Kuhusu udhamini wao kwa jukwaa la ‘Familia kitchen party Gala’, linaloandaliwa na Women Footprints Initiative, alisema wameamua kushirikiana nao kwa lengo la kupunguza vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi.Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment