Imeelezwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea wapo kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana,
mfamasia kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Goodluck Madehu,
alisema vijana wa umri huo hawana utaratibu mzuri wa kula na kufanya
mazoezi.
Madehu alisema hayo wakati wa mkutano wa 28 wa mwaka wa wanasayansi
na watafiti kutoka nchi mbalimbali duniani ulioandaliwa na Taasisi ya
Taifa ya Utafiti na Magonjwa (NIMRI) uliomalizika jana jijini hapa.
“Hili sasa linaweza kuwa janga la taifa maana kila tunakokwenda kutoa
huduma za kupima bila malipo kama ilivyo utaratibu wa NIHF, tunagundua
vijana wengi wana uzito uliozidi na uliopindukia.
“Inatokana na ukosefu wa elimu ya lishe, watu wanakula bila
mpangilio, wanashindwa kujizuia na mbaya zaidi hawafanyi mazoezi, hata
kwa macho mtu mwenye uzito uliozidi anaonekana…,” alisema mfamasia
huyo.
Kwa mujibu wa Madehu, NIHF imeamua kuwasaidia vijana na wananchi wote
kwa kuchapisha na kugawa vitabu vinavyoeleza namna sahihi ya kula na
kudhibiti uzito wa mwili.
Alisema uzito unaozidi na kupindukia unakaribisha maradhi yasiyoambukizwa, likiwemo shinikizo la damu, sukari na saratani.
Mfamasia huyo alisema kwa siku tatu za mkutano huo, NHIF imetoa bure
huduma za vipimo vya sukari, shinikizo la damu na urefu na uzito (BMI)
ambapo washiriki zaidi ya 260 kati ya 350 wa mkutano huo walihudumiwa
na asilimia 98 ya waliopima walikutwa na uzito uliozidi.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment