MENEJA wa Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni, Alune Kasililika
(28), anadaiwa kuchonga mpango wa majambazi kuvamia na kisha kupora
kiasi kikubwa cha fedha katika tawi hilo.
Katika tukio hilo lililotikisa Jiji la Dar es Salaam kwa takriban
wiki tatu zilizopita, majambazi hao kwa kushirikiana na meneja huyo,
wanadaiwa kuchota sh milioni 390. 2, dola za Marekani 5,5000, euro 2,150
na paundi 50.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa
Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema meneja
huyo mkazi wa Kimara, alikula njama na baadhi ya maofisa wake,
majambazi ambao kwa pamoja walifanikisha kupora fedha hizo.
Alisema kuwa Meneja Kasililika, msichana mwenye umri wa miaka 28,
alihamisha robo tatu ya fedha zilizoporwa siku moja kabla ya tukio na
kumkabidhi mumewe ambaye hadi sasa ametolokea nje ya nchi na siku ya
tukio la ujambazi ilikuwa sawa na kukamilisha sinema.
“Siku ya tukio ilikuwa kama sinema. Ilikuwa ni siku ya kutekeleza
uporaji huo kwani fedha nyingi zilichotwa siku moja kabla ya tukio na
sinema hiyo ilichorwa na meneja huyo,” alisema Kamanda Kova.
Kova alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa meneja huyo kwa
kushirikiana na mfanyakazi mwenzake ambaye ni Operesheni Meneja wa tawi
hilo, Neema Bachu, walikula njama na watu wengine wa nje kufanikisha
wizi huo.
Alisema uchunguzi huo pia unaonyesha kuwa meneja huyo na watu wake
walikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo.
Mbali na meneja huyo na ofisa wake, wengine ambao wanashikiliwa na
Polisi ni Frederick Lazaro (19), Kakamiye Julius (31) Idd Hamis (32),
Sezary Masawe na Boniface Muumba (29).
Watuhumiwa wengine ambao walipohojiwa walikiri kuhusika na kukutwa na
kiasi cha fedha ni Erasmus Mroto (38), Deo Olomy (32), Mohamed Athuman
(31), Joseph Mkoi (33), Lucy Amos (30) na Grace Amon (39).
Wizi huo ulitokea Aprili 15 mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi
katika tawi la benki hiyo baada ya majambazi hao kuwaweka chini ya
ulinzi watumishi wa benki hiyo na kupora fedha hizo.
Baada ya kupora fedha hizo, walikimbia kwa magari mawili, moja aina
ya OPA lenye namba za usajili T 421 BQV rangi ya fedha, ambalo pia
limekamatwa.
Wakati upelelezi wa tukio hili ukiendelea, polisi imewataka wananchi
waisaidie kwa kutoa taarifa ili kufanikisha kuwakamata waliohusika.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment