Hali ya kisiasa ya mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe imewekwa njiapanda baada ya Chadema kutangaza kumvua uanachama saa chache baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Zitto, ambaye amedumu kwenye nafasi ya ubunge kwa takriban mwaka mmoja kutokana na amri ya mahakama, sasa atalazimika kuamua kutangaza rasmi kujiunga na chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT) kama alivyokuwa amepanga kufanya wiki ijayo, au kukata rufaa mahakamani ili aendelee na majukumu yake ya kibunge hadi hapo muda muafaka utakapowadia.
Lakini mbunge huyo mwenye umri wa miaka 36, aliiambia Mwananchi muda mfupi baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake kuwa hakuwa na taarifa za kuwapo kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu jana na kwamba leo ataendelea kuchapa kazi za Bunge wakati atakapoiongoza Kamati ya
Hesabu za Serikali kupitia matumizi ya Shirika la Umeme (Tanesco).
Akitangaza kutimuliwa kwa Zitto, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kufungua kesi mahakamani, naibu katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema alikiuka katiba ambayo hairuhusu migogoro ya ndani ya chama kupelekwa mahakamani.
Alinukuu Sehemu ya Kwanza ya Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chadema, kipengele cha 8 (a) (X), inayosema: “Chadema itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama, wala hata siku moja haitashughulikia mambo kama hayo mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa kufuata taratibu na ngazi za chama hatavumuliwa na atafukuzwa uanachama.”
Lissu alisema Zitto alikiuka kipengele hicho kutokana na kufungua kesi Mahakama Kuu kushughulikia matatizo yake ndani ya chama.
Katika kesi yake Zitto, ambaye alikuwa naibu
katibu mkuu wa chama hicho, alikuwa anataka mahakama hiyo imwamuru
katibu mkuu wa Chadema ampe mwenendo na taarifa za vikao vya Kamati Kuu
vilivyomvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama.
Mbunge huyo pia aliomba na kufanikiwa kupata amri ya muda ya kuizuia Chadema, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili kuhusu uanachama wake, hadi hapo rufaa aliyokuwa anakusudia kukata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia amri hiyo ilizuia walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Zitto alifungua kesi hiyo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema.
Katika uamuzi wake jana, Jaji Richard Mziray ilitupilia mbali kesi hiyo na kumwamuru Zitto akilipe chama hicho gharama za kesi hiyo.
Jaji Mziray alijikita katika hoja mbili tu za pingamizi, akieleza kuwa kesi ilitakiwa kufunguliwa kwenye Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu badala ya Masjala Kuu ya Mahakama Kuu.Mwananchi
No comments:
Post a Comment