Kongamano hilo limeandaliwa na William Hague na Angelina Jolie
Viongozi wa kimataifa wanakutana jijini London kwa wiki nzima,
kwa kongamano la kumaliza dhulma za
kimapenzi katika mataifa
yanayokabiliwa na mizozo.Mkutano huo, wa siku nne umeandaliwa na Waziri
wa masuala ya nchi za kigeni wa Uingereza, William Hague na muigizaji
maarufu na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa, Angelina Jolie.
Kongamano hilo linajiri huku mataifa kadhaa barani Afrika
yakikabiliwa na changamoto ya kumaliza ubakaji unaotumiwa kama silaha ya
kivita.
Ni mwanzo wa kuidhinishwa kampeni ya miaka
miwili kutoa uhamasisho kuhusu kutumiwa kwa ubakaji na unyanyasaji wa
kimapenzi kama silaha wakati wa vita.
Waandalizi wa kongamano hilo wanasema wanataka
huu uwe wakati ambapo ulimwengu utazinduka na kutangaza kwamba
unyanyasaji wa kimapenzi sio jambo lisiloweza kuepukika wakati wa vita.
Uwajibikaji wa kimataifa
Tangu William Hague na Angelina Jolie wazinduwe
kampeni hiyo, mataifa mia moja na arobaini na nane yameidhinisha azimio
la uwajibikaji wa kumaliza unyanyasaji huo wa kimapenzi katika mizozo.
Lakini lengo sasa ni kuchukua hatua madhubuti, kuendeleza uchunguzi na kuripotiwa kwa visa hivyo vya unyanyasaji wa kimapenzi.
Pia katika kutoa usaidizi zaidi kwa waathiriwa na kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia unahimizwa katika operesheni za siku zijazo za kulinda amani.
Kiwango cha jukumu hilo ni kikubwa: katika miaka
ya tisaini, vita vya Bosnia vilisababisha kuwepo takriban waathiriwa
elfu hamsini wa unyanyasaji wa kimapenzi.
Takriban miongo miwili tangu vita hivyo vimalizike, ni wahalifu wapatao 60 pekee walioshtakiwa.BBC
No comments:
Post a Comment