Pages

Saturday, April 12, 2014

MWINJUMA AIBUKA NA DOUBLE M KAHAMA

 MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’ameiibua bendi yake ya Double M Sound na sasa itakuwa na makazi yake ya kudumu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwinjuma alisema ameamua kuifufua bendi hiyo na kutimkia Kahama, akiamini ndiko kwenye watu wanaopenda burudani na wenye fedha.

“Nimeifufua ghafla bendi ya Double M na kwamba nahamia mjini Kahama, sehemu ambayo ina malisho bora zaidi, ina hamasa na nimeona maisha ni popote nikiwa natafuta,” alisema.

Aliongeza kuwa bendi hiyo itakuwa na wanamuziki 14, wakiwemo waimbaji wa kike watatu watakaoleta ladha itakayofurahiwa na wengi.

Aliwataja wanamuziki hao kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe akisaidiana na Richard Magige, Sherri Abubakar ‘Shazi’ huku wanawake wakiwa ni Nana Mwashuya ‘Vampire’ na Furaha Mkwama.

Kwa upande wa solo na rhythm kutakuwa na Ally Akida ‘Tetenasi ya Geneva’, akisaidiana na David Shidodo, besi ni Said Bell, kinanda Paschal Kiinuka, tumba Hussein Ngalawa na Chocholi Mashine.

Mwinjuma pia alitangaza ratiba ya kuwapa burudani Kanda ya Ziwa, ambapo Aprili 18 watapiga Ukumbi wa Dream uliopo Kakola huku Aprili 19 watatumbuiza Ngara, Ukumbi wa City Center na Pasaka watakuwa Kibondo mkoani Kigoma katika Ukumbi wa FM Hall.

“Baada ya hapo tutaendelea na ratiba zetu kama kawaida Kahama, ambapo tutakuwa tukiendelea na mazoezi na hata kujiandaa kurekodi nyimbo zetu mpya,” alisema Mwinjuma

Aliongrza kuwa kwa kuanzia bendi hiyo itatumbuiza nyimbo zake nyingi za zamani zilizokuwa zikitamba, ukiwemo ule wa ‘Utafiti wa Mapenzi’.

Alisema pia atakuwa akifanya ziara katika nchi za Afrika Mashariki kama vile Uganda, Burundi na Kenya, lengo likiwa kuitangaza zaidi bendi hiyo.Tanzania Daima
.

No comments:

Post a Comment