Mbunifu mkongwe wa mitindo nchini, Asia Idarous, anatarajiwa kufanya
onesho la mavazi ya ubunifu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar, litakalofanyika Abuja, Nigeria, Aprili 25.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Idarous ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Fabak Fashions, alisema onesho hilo limeandaliwa na umoja
wa Watanzania waishio nchini Nigeria, ambapo usiku wa Aprili 25,
watakutana kwa pamoja na kufurahia miaka 50 ya Muungano, sambamba na
tafrija hiyo ya kipekee itakayowakutanisha magwiji wengine wa ubunifu wa
nchi hiyo.
“Nimefurahia sana kufanya onesho nchini Nigeria, bila shaka nitafanya
vizuri, kwani nina kila aina ya ubunifu wa mavazi likiwemo vazi la
khanga na mavazi mengine,” alisema Idarous na kuongeza kuwa kufanya
onesho hilo nchini humo, ni faraja kwake, kwani nchi hiyo kwa sasa
imekuwa ndiyo nchi tajiri katika bara la Afrika,
kutokana na uchumi wake
kukua maradufu huku ikiipiku Afrika Kusini iliyokuwa ikishikirla nafasi
ya juu katika uchumi.
Aliwataka Watanzania hasa wabunifu wa mitindo na wasanii, kubadilika
kwa kujikita katika kufanya kazi zenye tija kwa ukuaji wa uchumi kama
walivyofanikiwa Wanigeria.
Idarous ama Mama wa Mitindo, ni mkongwe wa mitindo hapa nchini,
ambapo amekuwa akiandaa maonesho mbalimbali ikiwemo ‘Usiku wa Khanga za
Kale’ na l‘Red in Lady’ kila mwaka nchini.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment