Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA), Dk. Sikubwambo Ngendabanka, amesema matumizi ya vipodozi vyenye
kemikali ni janga la kitaifa linaloisababishia serikali hasara ya
mabilioni fedha kutibu athari zake.
Wakati wa ufunguzi wa Wiki ya
Utumishi wa Umma iliyoanza Dar es Salaam jana, mkurugenzi huyo alisema
watumiaji wengi wa vipodozi hivyo ni wanawake.
Alisema kemikali zilizomo kwenye vipodozi hivyo zinasababisha
magonjwa ya ngozi na saratani ambayo matibabu yake yanagharimu fedha
nyingi zinazotolewa na serikali.
“Fedha za kuwatibu wagonjwa wa saratani kila mwaka ni nyingi
zingeweza kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo… ndiyo maana
nasema hili ni janga la kitaifa mama zetu wengi wanatumia wakitafuta
urembo kumbe wanakaribisha magonjwa,” alisema Ngendabanka.
Watumishi wa TFDA wanatumia maonyesho hayo kutoa elimu ya kubaini
bidhaa zilizo chini ya ubora, zilizokwisha muda wa matumizi na athari
za vipodozi vyenye kemikali kwa wananchi wanaofika katika banda hilo.
Maonyesho ya wiki ya utumishi yanafanyika kwenye viwanja vya Mnazi
Mmoja yakishirikisha idara, taasisi na mashirika ya serikali ambapo
wananchi wanapata fursa ya kujua shughuli zinazofanywa na serikali
kupitia maonyesho hayo yatakayohitimishwa Juni 23.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment