Mkazi wa Kigamboni, Baraka Mashauri (27) amedai kupigwa risasi katika
mguu wake kulia na askari polisi wa kituo kidogo cha Gymkhana, jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu tukio hilo, Mashauri alisema
lilitokea Mei 17 mwaka huu, saa saba mchana akiwa katika mtaa wa Shaban
Robert akipata chakula karibu na Mgahawa wa Holiday White akiwa na
mwenzake aliyemtaja kwa jina la Musa Mohamed.
Mashauri alisema kuwa baada ya muda mfupi lilitokea kundi la watu
wakimkimbiza mwizi ambaye alikamatwa na kupelekwa katika kituo hicho cha
polisi.
Alisema kuwa baada ya hapo, walitokea askari watatu waliokuwa
wamebeba silaha na walipomkaribia walimuita kwa jina lake kisha na
kuanza kumpiga risasi.
“Walinirushia risasi, kwa kuwa pembeni kulikuwa na mwenzangu
aliyejipumzisha, naye ilimpata ya pajani.
Risasi ya kwanza niliikwepa na
ndipo askari mmoja miongoni mwa wale watatu, Mohamed Shunda ambaye ni
OCS, alinipiga risasi huku akiniuliza ile simu aliyoiba yule mwizi iko
wapi.
“Wakati nikiwa nagaa gaa chini kwa maumivu, alikuja mtu akanieleza
kuwa yule mwizi kasema alimpa simu mtu aliyekimbilia maeneo ya Gymkhana
na baada ya hapo askari wale walinichukua kwa gari lao aina ya
Defender
na kuelekea kituo cha polisi cha Central, waliniacha kwenye gari na
baada ya muda wakaja na fomu ya matibabu (PF3) na kunipeleka Hospiatali
ya Muhimbili ambako waliniacha hapo huku wakiondoka na fomu
hiyo,”alisema.
Mashauri aliongeza kuwa baada ya kufika Muhimbili alipata matibabu na
kufungwa bandeji ngumu (POP) katika kidonda kilichotokana na risasi.
“Nilifikishwa saa 9 alasiri na nikatolewa Mei 18, lakini huu mguu
kama unavyouona siwezi kutembea, ndani unauma nahisi kuna vitu na sijui
hatma ya yangu itakuaje. Nimeandikiwa dawa ila fedha sina, ninadaiwa na
hospitali sijui naishije,”alisema.
Katika kutoa malalamiko yake, alifika katika Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC) na kuonana na mratibu wa kituo hicho aliyemtaja kwa
jina la Mkuta Masoli.
Tanzania Daima limeiona picha ya Xray inayoonesha namna risasi hiyo
ilivyopenya na kuvunja mfupa pamoja na uthibitisho wa vyeti
vilivyotolewa vikiwa vimesainiwa na Dk. Stephen wa Taasisi ya Mifupa
(MOI).
James Yustas, ambaye alimsaidia Mashauri kufika katika ofisi za
gazeti, juzi alijikuta matatani baada ya kukamatwa na polisi na
kupelekwa kituo cha kikuu na kuhojiwa sababu za kumpeleka mlalamikaji
katika vyombo vya habari na ofisi za LHRC.
“Nilikamatwa juzi na askari wakaniweka rumande ambako walichukua simu
zangu zote mbili lakini waliniachia jana saa moja asubuhi na kunitaka
niachane na suala hilo,” alisema Yustas.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alipoulizwa
kuhusu tukio hilo alisema hana taarifa nalo na hivyo kuomba waandishi
kumsaidia kumkutanisha na majeruhi huyo ili aende akatoe maelezo yake.
Alisema “siwezi kuzungumza chochote kuhusu tukio hilo kwa sababu
hakuna aliyefika kunilalamikia kuhusu tukio hilo, hivyo naomba kama
mnajua alipo mwambieni aje kulalamika,” alisema TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment