Watuhumiwa 14, wanaosadikiwa kujihusisha na makundi ya kigaidi
nchini, ikiwemo kundi maarufu la Al-Shabab, wamefikishwa mahakamani
kujibu mashtaka 16 ya kuua na kukusudia kuua.
Al-Shabab ni kundi la kigaidi la nchini Somalia, linaloendesha mauaji, utekaji nyara, uvamizi ndani na nje ya nchi hiyo.
Watuhumiwa hao, wanahusishwa na tukio la milipuko ya mabomu katika maeneo ya Mianzini na Arusha Night Park hivi karibuni.
Washtakiwa hao wanatuhumiwa kusajili na kusafirisha vijana kwenda
katika mafunzo maalum nje ya nchi kujifundisha masuala ya kigaidi na
kushawishi vijana katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wakisomewa mashtaka jana, katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha na
Mwendesha Mashtaka wakili wa serikali, Hariri Muda, mbele ya Hakimu
Mustapha Sian, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa
mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Waliofikishwa mahakamani jana ni Abdallah Athumani, Abdallah
Thabiti,Ally Hamisi, Abdallah Wambura,
Rajabu Hemedi, Hasani Saidi, Ally
Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa,Swalehe Hamisi,Abdallah Yasini,
Sudi Nasibu Lusuma huku washtakiwa wawili; Abdul-karimu Thabia Hasia na
Rajabu Phili Hemedi wakisomewa mashtaka yao wakiwa wamelazwa katika
Hospitali ya Mount Meru.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa serikali, Muda alidai upelelezi wa
kesi hiyo bado unaendelea na utakapokamilika kesi hiyo itahamishiwa
Mahakama Kuu kwa kusikilizwa.
Mwendesha mashtaka huyo, alidai kati ya mwaka 2010 hadi 2014,
washtakiwa hao walifanya kazi ya kushawishi na kusajili vijana kwa lengo
la kuwapeleka katika mafunzo maalum ya uhalifu katika nchi moja ambayo
jina limehifadhiwa kwa sasa.
Alidai katika muda huo walisajili vijana kutoka maeneo mbalimbali
nchini ambapo jitihada za uchunguzi kuwabaini wote waliosajiliwa
zinaendelea ili wakipatikana nao waunganishwe katika kesi hiyo.
Hakimu Siani aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 12, mwaka huu na kama
upelelezi utakakuwa umekamilika kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu.
Walivyopelekwa
Magari yasiyopungua 10 yaliyokuwa yamesheheni askari wenye silaha
ndiyo yaliyowapeleka mahakamani na kuwarudisha magereza watuhumia hao.
Msafara wa watuhumiwa hao pia ulikuwa ukiongozwa na pikipiki za
polisi zilizokuwa zikiliza ving’ora, hali iliyowafanya baadhi ya
wananchi kupata hofu.
Shughuli za mahakama nazo zilisimama kwa muda baada ya watuhumiwa hao
kufikishwa hapo na kuwekwa katika chumba maalum kabla ya kuingia ndani
katika ukumbi wa mahakama kusikiliza mashtaka yao.
Ndani ya ukumbi kulisheheni askari wenye silaha na askari Kanzu
waliovaa kiraia huku mbwa wa polisi nao wakirandaranda nje ya viunga
vya mahakama hiyo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Polisi wazungumza
Awali akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kamanda wa
Polisi mkoa wa Arusha Mkurugenzi Mkuu wa Makosa ya Jinai nchini (DCI),
Issaya Mungulu, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na
upelelezi ulioanza muda mrefu baada ya kuanza kutokea milipuko ya mabomu
jijini Arusha.
Alisema matokeo ya upelelezi huo ndiyo yaliyosababisha kukamatwa kwa
watuhumiwa hao na polisi inaelendelea kuwasaka wengine waliohusika na
milipuko ya mabomu katika jiji hilo.
Alisema watuhumiwa zaidi ya 25 ndiyo wanaodhaniwa kuhusika na
matukio hayo mawili na pindi watakapokamatwa nao watafikishwa
mahakamani.TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment