Msemaji wa maoni ya wachache katika Kamati namba 5, David Kafulila,
amesema makada wa CCM hawana hadhi ya kumtusi aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alisema Warioba amefanya kazi kubwa katika taifa hili kuliko baadhi
ya makada wanaomdharau, kumtusi na kukebehi maoni ya tume aliyokuwa
akiiongoza ambayo ilipendekeza muundo wa serikali tatu unaokinzana na
matakwa ya CCM inayotaka serikali mbili.
Wakati akitoa ufafanuzi huo, Kafulila alikuwa akishangiliwa na idadi
kubwa ya wajumbe, hasa kutoka vyama vya upinzani waliokuwa wakiimba
‘Kafulila kama Warioba, CCM wameliwa, serikali tatu hazikwepeki.’
Mjumbe huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi),
alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maoni ya
watu wachache wa kamati namba tano ambapo alisema hawana nia ya kuuvunja
Muungano bali kuuimarisha kwa kuleta mabadiliko ya serikali tatu badala
ya mbili za sasa.
Kafulila alisema Jaji Warioba anapingwa hata na watu wasiofanya jambo
lolote katika nchi wakati kiongozi huyo ameaminika tangu utawala wa
Mwalimu Nyerere mpaka wa Rais Kikwete aliyemteua kuongoza Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alisema takwimu zilizotolewa na tume ya Jaji Warioba, zimepingwa sana
kwakuwa zimewahoji watu 300,000 na waliotaka serikali tatu ni 17,000.
“Warioba si mtu wa level ya kutukanwa, kasimamia kile kilichosemwa na
wananchi, Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, wote walitoa
maoni ya kutaka serikali tatu, wanaomtukana wana level ndogo kuliko yeye
aliyefanya kazi kubwa katika nchi hii,” alisema.
Aliongeza kuwa anawashangaa hata wasomi wanaokosoa takwimu hizo
kwakuwa kilichofanyika ni kuchukua ‘sampling’ ambazo ndizo hutumika
katika tafiti mbalimbali zinazotoa matokeo yanayokaribiana na ukweli.
“Kweli nchi yetu inaelekea kubaya, yaani mlitaka Warioba afanye sensa
ili mridhike kuwa idadi ya waliotoa maoni ndiyo inayolingana wananchi
milioni 45 waliopo nchini? Usomi wa wapi huu?” alisema.
“Synovete walifanya utafiti mwaka 2005 waliwahoji watu kati ya
2,000-3,000 ambapo walitoa ripoti kuwa
Rais Jakaya Kikwete atashinda kwa
asilimia 80 na utafiti huo ulikuwa kweli ilipofika wakati wa uchaguzi,”
alisema.
“Kenya walifanya hivyo hivyo kwa kutumia watu 2,000-3,000 kuakisi
mawazo ya watu milioni 300, sasa kwanini hapa kwetu mnataka kusema
Warioba hakuwa sahihi?
“Wengi nyinyi mmesoma mnajua sampo ile ilikuwa sahihi, mnashindwaje
kuona maoni ya watu 17,000 ni kubwa zaidi kuliko ile inayohitajika?
Maoni ya tume ya Warioba ndiyo maoni ya wananchi, si yake, jambo lile
lilifanyika kwa tume mbalimbali wakaja na maoni yale yale ya kutaka
serikali tatu.
“Unapobaki kusimamia tatu ni kosa, utachemka, ni suala la muda tu,
wananchi wanatuona, tunaposema wao ni wachache nyinyi watu 600 wa humu
ndani mnapata wapi uhalali wa kutunga Katiba?
“Hoja hii mnaikataa kwakuwa inagusa masilahi yenu lakini zile
zilizotolewa na idadi ndogo kuliko ile ya muungano lakini hamhoji, hivi
kuna jambo gani hapa? Kama watu 17,000 ni wachache sasa inakuwaje nyinyi
600 muwe wengi kuliko wale waliotoa maoni?” alihoji.
Alisema makada wa CCM wanatumia mbinu zile zile walizozitumia kukataa mfumo wa vyama vingi kukataa serikali tatu.
Hivi hamna mbinu nyingine? Propaganda za leo kuwa serikali tatu
zitavunja muungano ni zilezile za kuwa vyama vingi vitaleta vita,
tuangalie mazingira, tujielekeze kubadili muundo wa muungano mapema kwa
utulivu na amani,” alisema.
Kafulila alisema muundo wa serikali mbili uliodumu kwa miaka 50,
umeonyesha una matatizo makubwa na umezusha malalamiko ya mara kwa mara
kutoka kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara ( Tanganyika ).
Alisema makada wa CCM, wanaomdhalilisha Warioba kwa rasimu waliyoitoa
kuruhusu muundo wa serikali tatu wanadai kuwa mfumo huo utakuwa na
gharama kubwa huku serikali ya shirikisho itakuwa ikiwategemea nchi
washirika kujiendesha.
Kafulila alisema Serikali ya Shirikisho haitakuwa na sababu ya
kutegemea mapato ya nchi washirika kama itakubalika mapato ya bandari
ambayo kwa mwaka ni sh trilioni 3.3 yatatumika kuendesha shughuli za
muungano.
Alibainisha kuwa wamefanya hesabu hizo na kubaini kuwa mapato hayo
ambayo ni asilimia 40 ya pato la taifa sasa yanatosha kuiendesha
serikali hiyo ambayo gharama zake hazitazidi sh trilioni tatu, hivyo
kiasi kilichobakia kitatumika kusaidia shughuli za maendeleo na
zinatosha kabisa.
“Hatuna lengo la kuharibu muungano bali kuuboresha zaidi, leo hii
mnakuja na hoja kuwa ikija serikali ya tatu upande mmoja wa muungano
(Tanganyika) ndiyo itakayobeba gharama hizo kwakuwa Tanganyika ina eneo
kubwa sana, ina rasilimali nyingi zaidi hivyo lazima itachangia fedha
nyingi zaidi. Anayechangia zaidi ana mahitaji makubwa zaidi.
“Tanganyika hivi sasa ndiyo inayobeba gharama katika mfumo wa
serikali mbili, lakini hamuizungumzi kwa nia mbaya, sasa kwanini
tunakataa gharama hizo kubebwa katika mfumo wa serikali tatu? Kuna kitu
gani hapa ambacho hakitaki kuwekwa wazi ili kila mmoja wetu afahamu
kilinachoendelea?” alihoji.
Kafulila alisema makada wa CCM wamekuwa wakitumia maneno ya hayati
Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kujibu mashambuilizi ya serikali tatu
wakati wanajua kiongozi huyo hakuwa nabii.
Alisema Nyerere alikuwa akifanya vitu kulingana na wakati husika
ndiyo maana mwaka 1965 aliufuta mfumo wa vyama vingi lakini mwaka 1992,
nyakati zilimfanya abadilike na kuwashawishi wenzake wakubaliane na
mfumo wa vyama vingi licha ya wengi kutoutaka.
Kafulila alisema vitisho vya vyama ndivyo vimechangia majadiliano ya
serikali mbili au tatu kuonekana magumu na pia yamewaumiza watu wengi.
“Nyinyi CCM, jambo hili mkiliacha litakuja kuwaumiza zaidi, huko
tuendako mtalazimika kutengeneza serikali tatu kwa mashinikizo huku
mkiwa hamna ‘control’ wala utulivu kama mlionao hivi sasa.
“Mtayafanya vibaya, kwa sababu ya mazingira tofauti na sasa huko muendako kutakuwa kubaya zaidi,” alisema.
Naye Suleiman Bungara, maarufu kwa jina la ‘Bwege’ alisema kwamba:
“Kwa hoja iliyowasilishwa leo na Kafulila, akichangia pale bungeni…CCM
wamekwisha. Hivi mtu gani atakubali kuwa na serikali mbili na nchi
mbili?”
Bwege ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kusini, alisema kwamba serikali tatu
hazizuiliki kwa mazingira ya sasa na kuhoji: “Anayebisha nina shaka na
utashi wake. Eeh ndiyo… kwa sababu tume zote, zile za Jaji Francis
Nyalali, Jaji Robert Kisanga na Jaji Joseph Warioba wote wamependekeza
serikali tatu, hawa wanaobisha sasa wana nini?” alihoji.
Hashim Rungwe, ambaye pia ni mjumbe wa bunge hilo kutoka Chama cha
Umma (CHAUMA), alisema mwanga umeanza kuonekana wa mwelekeo wa kupata
katiba ya serikali tatu, lakini bado ana wasiwasi wa utashi na wingi wa
wajumbe kutoka CCM ambao wana msimamo wa serikali mbili. Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment