Mmwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima mkoani
Mbeya, Gordon Kalulunga (35), amenusurika kifo baada ya kupigwa na
mgambo wa jiji hili waliokuwa kwenye shughuli za operesheni vunjavunja.
Kalulunga alikutwa na zahama hiyo wakati akipiga picha mwendelezo wa
operesheni hiyo iliyokuwa ikifanyika sehemu ambayo mtoto wa miezi minne
alifichwa na mama yake akiwa kwenye mfuko wa salfeti kabla ya kuokolewa
na wasamaria wema.
Vunjavunja hiyo ilifanyika wakati wa sherehe za Jumatatu ya Pasaka
baada ya uongozi wa jiji kubariki shughuli ya kuwaondoa wafanyabiashara
waliopanga bidhaa zao kando ya barabara kuu ya Tanzania – Zambia eneo la
Mwanjelwa.
“Nilikuwa kazini akatokea mwanamke amevaa gauni refu la rangi ya
njano na kunikaba shati, ndipo mgambo wa jiji walipokuja na kuanza
kunipiga… ilibidi kamera yangu nimkabidhi polisi. Lakini nimepoteza
redio yangu ya kurekodia,” alisema Kalulunga.
Alisema baada ya tukio hilo, ilibidi atoe taarifa kwenye kituo kidogo
cha polisi Mwanjelwa na kupewa fomu ya matibabu (PF3) kisha ilibidi
apatiwe matibabu na aliporudi polisi, alitakiwa na mkuu wa kituo akatoe
maelezo kwenye kituo kikuu cha polisi kwa OC –CID au mkuu wa polisi
wilaya (OCD).
“Namshukuru Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya, Richard Mchomvu ametumia
busara kunikutanisha na kiongozi wa operesheni hiyo kutoka idara ya
afya, mkuu wa mgambo na bosi wangu, jiji wamekiri kunipiga kwa madai ya
kutofahamu kuwa ni mwandishi,” alisema Kalulunga.
Kwa upande wake, Mchomvu aliushauri uongozi wa jiji hilo kushirikiana
na vyombo vya habari katika majukumu yake kwa kuwa wananchi wanapaswa
kuelimishwa zaidi kila jambo linapofanyika na kusisitiza kuwa usafi wa
jiji ni muhimu, hivyo kila upande una jukumu lake.
Wakati hayo yakitokea, wauzaji magazeti jijini humo wamelalamikia
operesheni hiyo baada ya meza zao kuvunjwa usiku wa manane wakati
uongozi wa jiji hilo unafahamu fika aina ya meza zilizoruhusiwa kuwepo
kwa ajili ya kuuzia magazeti.Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment