Pages

Thursday, April 24, 2014

MUHONGO AWATANGAZIA KIAMA WAZEE

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametangaza kiama kwa watumishi wazee na kukaribisha vijana wenye elimu kushika nyadhifa za juu katika wizara hiyo.
Waziri huyo alisema elimu ya chini kwa mtumishi wa wizara yake kuanzia mhudumu itakuwa shahada ya pili ili kwenda na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia duniani.


Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo mjini hapa jana, waziri huyo alisema kuwa tangu alipoingia wizarani hapo, amepata malalamiko mengi ambayo hayafanyiwi kazi kutokana na  uduni wa elimu waliyonayo baadhi ya wafanyakazi wake ambao wengi ni wazee.

Waziri Muhongo, pia ametangaza kiama kwa watumishi na watendaji wa wizara hiyo waliojipatia vitalu vya madini kwa njia sizizo halali, ikiwemo kutumia majina bandia na kumuagiza Kamishna wa Madini nchini, Paul Masanja, kukusanya majina yao ili washughulikiwe kabla ya kikao cha Bunge la Bajeti kinachotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.

Waziri huyo ametoa miezi sita kwa wakurugenzi wa sekta ya Nishati na Madini kumpa orodha ya watumishi wavivu na wanaoharibu wizara hiyo kwa kuendekeza rushwa na ubinafsi.

“Kwa kuanzia, nataka wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu, mje na majina ya wazembe na mpango mkakati unaopima ufanisi wa kila mtumishi kuanzia wizarani hadi ngazi ya chini, vinginevyo jiandaeni kuondoka. Hatuwezi kuwa kila mwaka hali ni ile ile iliyojaa mikakati isiyo na ufanisi,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Waziri Muhongo alisema amechoshwa na mtindo alioukuta wizarani hapo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu wizara yake, lakini hayafanyiwi kazi kutokana na uduni wa elimu hasa wa watendaji wazee wizarani hapo.

Huku akiwasimamisha mara kwa mara Kamishna wa Madini, Paulo Masanja na wakurugenzi wa wizara hiyo kujibu baadhi ya matatizo, Profesa Muhongo alisema muda wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha kwani wizara hiyo inakua kwa kasi hasa baada ya ugunduzi wa mafuta na gesi.

Aliwashukia wanasheria katika wizara hiyo kuwa chanzo cha kuliingiza taifa kwenye matatizo kwa kusaini mikataba isiyo na tija uchochoroni na nje ya nchi.

“Kuanzia sasa ni marufuku kusikia eti umeitwa kwenda nje ya nchi kusaini mkataba wowote unaohusu rasilimali za nchi, mikataba yote itasainiwa nchini na kwenye ofisi za wizara au mahali palipoandaliwa na sisi wenyewe, kama kuna mtu anataka kujaribu kuona nini kitatokea ajaribu,” alionya.

Aliongeza kuwa fedha nyingi zinapotea kutokana na uzembe wa wanasheria na kusababisha wizara kuchangia kiasi kidogo cha asilimia 3.5 kwenye pato la taifa wakati sekta ya nishati na madini inakua kwa asilimia 15.

Kuhusu nishati, aliitaka Tanesco kufanya tathmini kuondoa mianya ya rushwa kabla hajaamua kulisafisha shirika hilo kwa mara nyingine.

“Hili nalisema bila chenga, sina huruma na mtu asiyeridhika na ninachomlipa, kama hawezi aondoke haraka kabla hajachafuka. Kumbukeni hata mimi nimeviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kufuatilia nyendo zangu popote, hatuwezi kuwa ombaomba kila kukicha wakati tuna rasilimali nyingi,” alisema Profesa Muhongo.

Waziri Muhongo aliwataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi kujiwekea malengo yanayotekelezeka, wakizingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2015 kwa kuongeza watumiaji wa nishati ya umeme kutoka asilimia 24 hadi zaidi ya asilimia 34 ya kimataifa.

Alisema wizara yake itakuwa karibu na wachimbaji wadogo kwa kuwaandalia utaratibu wa kupata mikopo yenye masharti nafuu ambapo sh bilioni 2.5, zitatengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili hiyo.

Kuhusu soko la madini duniani, Waziri Muhongo aliwaeleza wajumbe wa baraza hilo kuwa limeshuka kiasi cha kusababisha wawekezaji wa madini kupunguza kasi ya kuanzisha migodi mipya nchini.

Akijibu baadhi ya madai Kamishina wa Madini, Masanja alimfahamisha Waziri Muhongo kuwa kazi ya kuhakiki majina ya watumishi na wafanyakazi wazembe na wenye vitalu vya madini itakamilika Julai na atayawasilisha ofisini kwake kwa hatua zaidi.Tanzania Daima


No comments:

Post a Comment