Watu kadha wameripotiwa kuuawa nchini Nigeria kutokana na milipuko
miwili iliyotokea katika kituo cha mabasi katika mji mkuu wa Nigeria,
Abuja.
Mwandishi wa BBC mjini Abuja, Haruna Tangaza anasema milipuko hiyo
ilitokea wakati abiria wakiwa katika harakati za kupanda mabasi na teksi
wakienda maofisini katikati ya mji wa Abuja.
Watu walioshuhudia tukio hilo wanasema miili ya watu imetapakaa katika eneo la tukio.
Waandishi wa habari wanasema huenda tukio hili ni shambulio la kikundi cha wapiganaji wa Kiislam kijulikanacho kama Boko Haram.
Mmoja wa walioshuhudia mlipuko huo, Badamsi
Nyanya ameiambia BBC kuwa ameona miili 40 ikiondolewa. Watu wengine
walioshuhudia tukio hilo wanasema wamewaona wafanyakazi wa uokoaji na
polisi wakiokota sehemu za miili zilizotawanywa na milipuko hiyo.
Mlipuko huo ulichimba chini mita 1.2 katika viwanja vya Nyanya Motor
Park, kiasi cha kilomita 16 kutoka katikati ya jiji, na kuharibu zaidi
ya magari 30, na kusababisha mlipuko zaidi kutokana na matangi ya mafuta
ya magari hayo kushika moto na kuwaka.
Magari ya wagonjwa yamekuwa yakibeba miili ya watu waliokufa na wale waliojeruhiwa katika hospitali za karibu.
Shuhuda mwingine Bi Mimi Daniels, ambaye
anafanya kazi mjini Abuja, anasema: "nilikuwa nasubiri basi niliposikia
mlipuko mkubwa halafu nikaona moshi," ameiambia Reuters.
"Watu walikuwa wakikimbia ovyo kutokana na taharuki."BBC
No comments:
Post a Comment