Pages

Monday, March 24, 2014

NKAMIA:NITAFUNGIA NA KUFUTA MAGAZETI



VITISHO vya watendaji wa serikali kwa vyombo vya habari vimezidi kushika kasi, safari hii Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Juma Nkamia, akitishia kuvifungia au kuvifuta.

Nkamia amebainisha kuwa magazeti yanayowachafua watu, serikali na kuhatarisha usalama wa nchi yatakumbana na kifungo.

Itakumbukwa mwaka jana serikali ililifungia gazeti la Mtanzania kwa miezi mitatu na Mwananchi kwa wiki mbili, kwa madai ya kuandika habari za kichochezi.

Nkamia, alitoa vitisho hivyo  jana jijini hapa  kwenye tamasha la vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Voice of Youth (VOYC) lililokuwa likijadili masuala mbalimbali yahusuyo vijana.

Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakijadiliwa ni ujira, uzalendo, ujasiriamali na ajira,
Nkamia alisema hatakubali siku moja asutwe kwa kutotimiza wajibu wake katika wizara anayoisimamia, kwa kuwaachia waandishi wasiofuata maadili ya taaluma yao.

“Mimi sitaki kufanya kazi na waaandishi wa habari makanjanja, ambao si makini na wanaofanya kazi kwa masilahi ya kundi fulani la watu.

“Tutakifuta, kukifungia chombo chochote cha habari pamoja na waandishi wake wanaokwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari, sitaruhusu wanaoendekeza kuwachafua wengine, umbea,” alisema.

Alisema amefanya kazi hiyo kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo kabla ya kuingia kwenye siasa ambako sasa anasimamia wizara inayoshughulika na waandishi wa habari.

Nkamia pia alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana waache kushiriki kwenye maandamano yanayoitishwa na vyama vya siasa alivyoviita havina malengo mema kwa taifa.

Alibainisha kuwa vijana hawawezi kupatiwa fedha kama hawafanyi kazi yoyote, kwani hata mataifa yaliyoendelea ambayo ni Marekani na Uingereza hawafanyi hivyo.

Hata hivyo katika mkutano huo, viongozi wa halmashauri na mkoa walikacha kuhudhuria na hawakutuma wawakilishi katika tamasha hilo licha ya kualikwa.

Kukacha kwao huko kulisababisha gumzo kubwa na Afisa Tarafa ya Nyamagana, Maximilian Kailanga, alibeba jukumu la kumkaribisha Nkamia.UDAKU


No comments:

Post a Comment