MKARIBISHE
ROHO MTAKATIFU. *Rum 8:26-27 *Yoh 14:16-17
Yesu
alisema Roho Mtakatifu ni msaidizi wetu. Atatusaidia na kutufundisha yote, kwa
maana pasipo yeye, sisi hatuwezi neno lolote. Na sisi peke yetu hatujui kuomba
ipasavyo, bali yeye (Roho) ajua kutuombea kwa Mungu kama vile Mungu apendavyo.
Hivyo kabla ya kuanza maombi au kusoma neno au ibada au safari au mitihani au
kikao n.k. jifunze kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, uombe msaada wake, akupe
ufanisi/ubora katika yote yakupasayo kufanya.
Tambua
Utu wake, Uungu na Uweza wake.
Jikabidhi
katika Nguvu ya Uongozi wake.
Tii
kila Uongozi anaokupa.
FANYA TOBA NA UTAKASO. *Isa 59:1-2,
Yoh 9:31, 1Yoh 1:8-9,7
Sikio la Bwana si zito kusikia wala mkono wake si mfupi
kushindwa kututendea mambo tumwombayo, bali maovu yetu ndiyo yanatufarakanisha
na Mungu wetu. Mungu hawasikii wenye dhambi. Hivyo chukua muda wa kutafakari na
kuungama dhambi zako mbele za Mungu na kuzitubu kwa kumaanisha kuziacha. Mungu
ni mwaminifu kutusamehe na kututakasa na uchafu wote. (Isa 1:18). Lakini, kabla
hujafanya toba yako binfsi;
(i)
- Kwanza, samehe wote waliokukosea,
hata kama hawajaja
kukuomba msamaha. Usipowasamehe
waliokukosea, na Mungu
hataweza kukusamehe wewe. (Math
6:12,14-15)
(ii) - Ndipo nawe ufanye toba yako
binafsi. Na Mungu
atakusamehe kabisa.
Hata kama ni
nyekundu sana, zitakuwa nyeupe sana. (Isa 1:18, Isa 43:25)
3. MSIFU, MUABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Zab 147 na Zab 148
Msifu Bwana kwa Matendo yake makuu, mwabudu Bwana kwa uzuri
wake na kwa sifa zake. Mwadhimishe Mungu kwa Tabia zake, wema wake, fadhili
zake na baraka zake mbalimbali anazotutendea. Sifa yako ikifika vizuri mbele za
Mungu, ndipo atakuwa tayari kukupa haja za moyo wako. Haja zetu zimefichwa
nyuma ya mgomgo wa sifa. Ndio maana Neno linasema;
‘Nawe utajifurahisha kwa Bwana (kwa
kumsifu, kumwabudu na kumshukuru), naye atakupa
haja za moyo wako’ (Zab37:4).
Yesu anatuonyesha mfano; angalia sentensi yake ya kwanza
katika kuomba kwake imekuwa “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.”
(Math 6:9). Anaanza maombi kwa kumsifu Mungu. Msifu Mungu kwa kuimba na kwa
kunena/kusema/kuelezea. Mungu anataka kusifiwa na kutukuzwa. Ukifanya sifa
nzuri, ya kuufurahisha moyo wake, atakupa hata na vile ambavyo
hukutegemea/hukuomba.
4. MWELEZE MUNGU MAHITAJI NA HOJA ZAKO. *Wafilipi 4:6-7,19 Isa
43:26
Mweleze Mungu
zile hoja zilizokusukumwa kwenda kumwomba. Nenda mbele za Mungu kama ‘kuhani’
(1Pet 2:9). Kwa
unyenyekevu na heshima. Lakini kabla ya kumweleza mahitaji yako binafsi;
(i) Kwanza fanya ‘maombezi’ – ombea watu
wengine; (1Tim 2:1-4)
Viongozi mbalimbali na wenye mamlaka, watumishi wa Mungu,
marafiki zako, wenye shida, ndugu zako, nchi yako, shule yako, shirika lenu,
ofisi yenu, chama chenu, n.k. Usianze kujiombea mwenyewe tuu, zoea
kuwatanguliza wengine.
(ii) Kisha fanya ‘maombi yako’– ombea
haja za moyo wako. (Math 7:7-11)
Mweleze Mungu haja zako. Ongea na Mungu kwa uwazi na ukweli.
Japo anazijua haja zetu, lakini ameagiza kuwa tumwombe ndipo atafanya. ‘aombaye
hupokea’ yaani; asiyeomba, hapati. Mungu anasema tumpelekee hoja zenye
nguvu (Isa 41:21). Omba vitu vizuri na mambo makubwa ili upewe (pray for good
things and big things)
5. FANYA MAOMBI YA VITA VYA ROHONI. *Efe 6:10-13 *2Kor 10:3-5
Baada ya kumwendea Mungu na kumweleza mahitaji yako, sasa
simama kama ‘mfalme’, kwasababu wewe ni ‘mfalme’ (Ufu 5:8), tumia mamlaka yako
ya kifalme, ongea na hali/hitaji ulilokuwa unaliombea, na kwa mamlaka, amuru
iwe kama vile ulivyoomba/unavyotamani. Ndio maana Bwana Yesu alipokabidhiwa
mamlaka yote na Mungu, naye akatukabidhi sisi (kanisa lake) “Tazama,
nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Wala hakuna
kitakachowadhuru” (Luk 10:19, Yer 1:10, Yak 4:7). Tuma neno lenye mamlaka
katika hali/jambo ulilokuwa unaliombea, Amuru iwe vile ulivyokuwa unamwomba
Mungu iwe. Kemea kila roho ya shetani inayoweza kuwa inasababisha tatizo katika
swala lako.
6. OMBEA ULINZI JUU YA ULIYOYAOMBEA. *Math 6:13a
Baada ya kupiga vita vya kiroho, weka ulinzi katika yale
uliyoyaombea, ili shetani na mapepo yake wasiweze kuirudia hali/jambo/mtu yule
uliyemkomboa kwa maombi ya vita. Yesu alisema shetani akifukuzwa mahali, haendi
mbali, anasubiri kuona kama atapata upenyo wa kuparudia mahali pale alipokuwa
kwanza. (Math 12:43-45). Kwahiyo, usipoweka ulinzi, kuna uwezekano wa adui
kurudi na kuliharibu zaidi lile jambo uliloliombea na kulipata.
Kumbuka, unapoomba vizuri, unapokea papo hapo (katika
ulimwengu wa roho), lakini udhihirisho wake katika ulimwengu wa mwili, unaweza
kuchukua muda fulani. Hivyo katika muda huo wa kusubiri, shetani anaweza
akapita na kuzuia au kuharibu kile unachokisubiri kidhihirike katika ulimwengu
wa mwili. Ndio maana Yesu alitufundisha kuombea ulinzi, “tuokoe na yule
mwovu” (Math 6:13a). Weka ulinzi juu ya mambo yako yote. Jengea wigo wa
moto wa mbinguni (2Fal 6:16-17), Yafunike kwa damu ya Yesu na agiza malaika
walinzi walinde mambo yako masaa yote. Omba hivyo kila siku. (Zab 34:7, Zab
91:9-11, Ebr 1:13-14)
MSIFU, MWABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU.
*Math 6:13b
Yesu alianza maombi kwa kumsifu Mungu na kumtukuza. Na
akamaliza maombi yake kwa kumtukuza Mungu tena. Akasema “kwa kuwa ufalme ni
wako, na nguvu ni zako, sasa na hata milele” akamaliza. Kwahiyo nawe
kwa kumaliza maombi yako, msifu na kumshukuru Mungu tena, kwa ukuu wake,
uaminifu wake, na ahadi zake juu yetu. Ndipo ufunge maombi yako.
MUHIMU: TUMIA MAANDIKO KATIKA KUOMBA *Kol 3:16
-Katika kuomba
kwako, mara zote tumia maandiko kumkumbusha Mungu ahadi zake .(Isa 43:26).
Mungu analiangalia neno lake ili alitimize. Sababu pekee itakayomfanya Mungu
akupe alichoomba, ni ili kulitimiza neno lake. Hivyo, baada ya kumweleza
unachohitaji (kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu unayemwombea) mpe Mungu
andiko/neno lake linalokupa wewe uhalali wa kuomba hicho kitu mbele zake na
kupewa.
-Hata unapompinga na kumkemea shetani, baada ya kutoa
amri yako dhidi yake, shetani atasubiri kusikia andiko/neno linalomnyima yeye
uhalali wa kushika alichoshika. Ndio maana Yesu alimshinda shetani kwa neno la
Mungu. Alisema “imeandikwa” na shetani akashindwa. “Nao wakmshinda (shetani)
kwa damu ya Yesu na kwa Neno” (Ufu 12:11)
MBINU ZA
KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI KWA MUDA MREFU
1. CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU.
*Mk 1:35
ili
uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri
patakapokupa utulivu katika kuomba
(concentration in prayer). Ndio maana Mungu
alipenda kuongea na Musa juu ya
mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda
kuombea mlimani, mahali palipo mbali
na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani.
(Math 14:22-23). Tafuta mahali
patulivu; chumbani, kanisani, mlimani (Math 6:5-6)
2. CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7
Ili uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao
akili yako ma mwili
wako viko fresh. Usilazimishe kuomba
hata kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake.
Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali wa kupumzika. Usilazimishe
ratiba. ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri baadaye. Usije
ukajikuta unamkemea Yesu badala shetani. Penda kuomba wakati una nguvu ya akili
na mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana Yesu
alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. (Mk 1:35, Luka 4:42)
3. OMBA KATIKA
ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe 6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine
nzuri ya kuomba kwa muda mrefu na kwa ufanisi, ni kuomba kwa Roho; yaani kuomba
kwa kunena kwa lugha. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, Mungu anasikia pia,
lakini maombi yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu akili ya mtu haijui
kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba
kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Mk 16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)
4. OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE.
*Math 6:16-18
Kufunga kula kunasaidia kudhoofisha
mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu
siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili ukiwa umeshiba, unakuwa na
uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu mojawapo ya kuudhibiti, ni
kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili ukidhoofika kiasi, roho yako
inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab 35:13). Mashujaa wote wa imani
walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu anasema ‘mfungapo’ akimaanisha ratiba ya
kufunga, ipo. Inasaidia.
5. OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER).
*Mhu 4:9-10
Neno la Mungu
linasema, ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki
yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba
zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya
kiroho inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja,
bali wakiwa wawili, wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi! Shangaa! (Kumb
32:20) Hiyo ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka,
nguvu ya Mungu huongezeka.
Kwahiyo, wakati
mwingine, omba na rafiki yako, unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako
ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki wa kiroho. (Prayer
Partners). Kwa Mfano:- Math 17:1-9
Musa - alikuwa na Joshua, Haruni na
Huri
Eliya - alikuwa na Elisha
Daniel - alikuwa na Shadrack,
Meshack na Abednego.
Yesu - alikuwa na Petro, Yakobo na
Yohana.
Paul - alikuwa na Barnaba, Timotheo
na Tito.
Wewe Je? Uko na
nani katika urafiki wa kiroho?
Kama huna
rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichaglia. Tulia umwombe Mungu
akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye katika
roho, hata kama mmetengana kijiografia, lakini katika roho, mko na umoja mzuri
wa imani. (Math
18:18-19)
6. OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU
NA NGUVU ZAIDI.
Katika kuomba kwa muda mrefu, mkao
uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu. Yakupasa kujua nguvu yako na udhaifu
wako (strong point and weak point). Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha
haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi. Kwa Mfano:- Ukiwa umechoka,
usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea kitandani. Ni bora uombe
ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka usingizi na uchovu. Waombaji
hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi marefu. Wengine hawana mikao
maalum, bali wakiwa katika maombi, huwa wanabadilisha-badilisha mikao ili wasichoke.
Hiyo ni mbinu nzuri pia.
Mifano ya Mashujaa wa imani;
Ibrahim – aliomba kwa kusimama (Mwa
18:22)
Daniel - aliomba kwa kupiga magoti
(Dan 6:10)
Paul - aliomba kwa kupiga magoti
(Efe 3:14)
Yesu - aliomba kwa kulala chini
(Math 26:38-39)
Eliya - aliomba kwa kukaa chini na
kuweka kichwa
kati ya miguu (1Fal 18:42)
Mimi - huwa napenda kuomba kwa
kutembea tembea
Naweza kumaliza kilomita nyingi
chumbani kwangu
Nikitembea huku nikiomba.
Wewe Je?
Unaujua mkao wa nguvu? Kama
hujui, Tafuta kujua.
OMBA NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU
MUNGU.
Muziki wa kiroho, na wataratibu,
unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu. Muziki
wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee. Neno linasema, waimbaji
na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja, utukufu
wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani hawakuweza tena
kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa sifa,
ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga kinubi alipopiga
kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokija juu yake, naye
akatabiri.
Najaribu
kukuonyesha, kuna connection kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu.
Kwahiyo, ukiweza kuomba huku umeweka kanda au CD ya nyimbo za kiroho za
taratibu, utapata (experience) hamasa ya kiroho (motivation) na utasikia una
nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama unaweza, tengeneza kanda au CD maalum
yenye nyimbo nzuri unazozipenda wewe, ili uwe unaipiga wakati wa maombi.
Utajikuta unaweza kuomba kwa muda mrefu na kwa bubujiko zuri zaidi
Mwl. Mgisa Mtebe,Bsc Economics
Mzumbe University,+255 713 497 654
mgisamtebe@yahoo.com
No comments:
Post a Comment