1 Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.
2 Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua.
3 Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi.
4 Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia.
5 Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.
6 Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.
7 Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.
8 Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.
9 Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.
10 Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake;
11 Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.
12 Kwa maana aliyetukana si adui; Kama
ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama
ndivyo, ningejificha asinione.
13 Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.
14 Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.
15 Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.
16 Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa;
17 Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.
18 Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi.
19 Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu.
20 Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake.
21 Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.
22 Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.
23 Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha,
Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya
siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe.
No comments:
Post a Comment