Pages

Thursday, April 17, 2014

SHUGHULI YA UOKOAJI INAENDELEA KOREA KUSINI

Shughuli ya uokoaji wa abiria waliokuwa ndani ya ferry iliyozama jana Korea kusini imeingia siku yake ya pili hii leo maafisa wakiendelea kutafuta takriban abiria 289 waliokuwa ndani ya ferry hiyo ambao kufikia sasa hawajulikani walipo.

Vyombo vya uokoaji na wanamaji wa Korea wamekesha wakijaribu kuwaokoa abiria wa ferri hiyo inayosemekana ilikuwa imewabeba abiria 460 asilimia kubwa ikiwa ni wanafunzi wa shule za upili waliokuwa wakienda kwa safari maalum ya masomo kuelekea kisiwa cha Jeju, nchini humo.

Baadhi ya walionusurika wamekuwa wakielezea hali ilivyokuwa ya kutisha ndani ya meli ilipoanza kusimama na kuyumba, ikiegemea upande mmoja na haraka kuanza kuzama. 
"Kwa kweli kulikuwa na sauti kubwa na meli ghafla ikaanza kuegemea upande mmoja," amesema abiria aliyeokolewa, Kim Song-Muk.

"watu walikuwa wakihangaika kukimbilia maeneo ya juu ya meli, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na meli kupinduka."
Hadi kufikia sasa haijafahamika kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo.

Kiongozi wa Kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Korea Kusini amesema abiria wapatao mia tatu hawajulikani walipo baada ya wengine 164 kuokolewa .
Watu saba pekee ndio wamedhibitishwa kufariki kufikia sasa.

Afisa mwingine amesema kuwa matumaini ya kuwapata wakiwa hai manusura inaendelea kudidimia
''Kuna matumaini ya kuwa fery hiyo ilipopinduka labda ilinasa hewa na hivyo labda abiria wanaweza kuwa hai lakini itakuwa vigumu

kuwapata wangali hai kwani meli hiyo ilipinduka kabisa na kufanya shughuli ya uokoaji kuwa ngumu.
Isitoshe kiwango cha joto cha maji ya bahari cha nyuzi 12 pekee ni hatari kwa maisha ya wahasiriwa ambao wamekesha ndani ya maji'.'
Jamaa za wahasiriwa wa mkasa huo walimfokea waziri mkuu wa Korea Chung Hong-won alipozuru eneo la uokozi .

Msemaji wa kampuni inayomiliki ferry hiyo Kim Young-boong, amewaomba radhi jamaa ya wale wote walioathirika katika mkasa huo.BBC

No comments:

Post a Comment