Pages

Thursday, March 20, 2014

MAHAKAMA YARUHUSU MKENYA KUFIKISHWA ICC


                                        Mahakama yaruhusu Mkenya afikishwe Hague

Mahakama kuu nchini Kenya imepinga agizo la kutokamatwa kwa mwandishi Walter Baraza baada ya
wakili wake Kibe Mungai kushindwa kufika mahakamani ili kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Hatua hiyo inamaanisha kwamba waziri wa usalama nchini Kenya Joseph Ole Lenku anaweza kuomba agizo lakukamatwa kwa mwandishi huyo kabla ya kuwasilishwa katika mahakama ya ICC anakotakikana.

Walter Baraza anatakikana na mahakama hiyo kwa madai ya kuingilia ushahidi katika kesi inayomkabili makamu wa raiswa kenya William Ruto.

Uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Richard Mwongo ni pigo kubwa kwa Mwandishi wa habari Walter Barasa, ambaye alikuwa aking'ang'ana kuhakikisha kuwa hakamatwi na kusafirishwa hadi Hague kushtakiwa  kwa kosa la kuwaingilia mashahidi waliokuwa wameorodheshwa na kiongozi wa Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Mwaka uliopita Kiongozi wa mashtaka katika The Hague, Fatou Bensouda, alitoa ombi ambalo lilikubaliwa na kuwasilishwa nchini Kenya ambapo ilitakiwa Waziri wa Maswala ya Usalama Nchini Kenya Joseph Ole Lenku, amkamate na kumfikishakatika The Hague.

Katika agizo hilo ilidaiwa kuwa Bwana Barasa alitumia pesa kuwahonga mashahidi waliotarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang.

Wakenya hao wawili wameshtakiwa kuwa walichangia pakubwa katika kuchochea ghasia za baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007 na 8, ambapo zaidi ya watu 1,300 waliuawa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya upande wa upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi.

Tangu kutangazwa kuwa akamatwe Baraza alikanusha kuwa alihusika katika njama hiyo na akadai kwamba Mahakama ya Kimataifa ilikuwa ikitaka kumgandamiza tu kwa sababu yeye alikataa kujitolea kutoa ushahidi dhidi ya Bwana Ruto na mwenzake Bwana Sang.

Awali Jaji Mwongo alikuwa ametoa amri kuwa Baraza akamatwe na kupelekwa Hague lakini Wakili wa Bwana Baraza Kibe Mungai, akaomba utekelezaji wa uamuzi huo uahirishwe ili yeye, Bwana Kibe ajitokeze mahakamani kutoa ushahidi kwa nini Bwana Baraza asikamatwe.

Wakili Kibe alitarajiwa kuwasilisha sababu zake jana lakini hakuwepo, jambo ambalo lilimlazimisha jaji kurejesha amri ya awali kuwa Baraza akamatwe.

Tangu mashtaka kuwasilishwa dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, naibu wake William Ruto na Bwana Sang katika Mahakama ya Kimataifa mashahidi wengi wamejiondoa kutoa ushahidi wakidai kuwa wanatishwa ingawa Bi Bensouda kwa upande wake anasema wengi wao wanahongwa na wandani wa washtakiwa.BBC

No comments:

Post a Comment