Pages

Tuesday, March 25, 2014

WATAKAO PAMBA TAMASHA LA PASAKA 2014

KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi wake Alex Msama, ipo katika maandalizi ya nguvu ya Tamasha la kimataifa la muziki wa Injili la Pasaka linalofanyika kwa mara ya 14.
Tamasha hilo ambalo litazinduliwa Aprili 20 katika Uwanja wa Taifa kabla ya kuhamia mikoani, tayari limekuwa gumzo kubwa si tu kwa wapenzi na wadau wa muziki wa Injili, hata kwa waimbaji waliothibitishwa kushiriki tamasha hilo.
 
Msama, Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo anasema waimbaji waliothibitishwa, wameanza kujifua ili kuwapa wapenzi na mashabiki wa tamasha hilo burudani ya nguvu kwa kadiri watakavyojaaliwa.
 
Waimbaji waliothibitisha ni Rebecca Malope na Kekeletso Phoofolo ‘Keke’ (Afrika Kusini), Faraja Ntaboba (DR Congo), Sara Kierie  (Kenya), Rose Muhando, Pendo Kilahiro na Upendo Nkone (Tanzania) na Ephraem Sekeleti wa Zambia.
 
1. Rebecca

Mwimbaji huyo aliyezaliwa mwaka 1968, alianza safari ya kulitangaza neno la Mungu kupitia kipaji cha uimbaji mwaka 1986.
 
Akiwa na umri wa miaka 18, yeye na dada yake Cynthia walihama kijijini kwao Lekazi na kuhamia karibu na mji wa Nelspruit kabla ya kusogea hadi katika mji wa Everton na mwishowe Jiji la Johannesburg.
Licha ya Rebeca kufanya hivyo katika kusaka ahueni ya maisha, pia ndani yake kulikuwa na msukumo wa kipaji cha uimbaji ambacho mwishowe kimewagusa wengi kiasi cha kukubalika na mamilioni ya watu.
 
Pengine kwake ilikuwa ni safari ngumu katika maisha yake, akijikuta akihama kutoka sehemu moja hadi nyingine, lakini sasa ni malkia wa muziki wa Injili Afrika kupitia kazi zake zenye mvuto na mguso wa aina yake kupitia albamu zake 32.
 
Hizo ni albamu alizofyatua katika kipindi chake cha miaka 27 ya huduma ya uimbaji ambapo mwaka 2009, alitoa albamu yake ya 30 iliyobebwa na jina la ‘My Hero’ na mwaka 2010, alitoa albamu ya 31.
Machi 14, 2011, ndipo Rebeca alifyatua albamu yake ya 32, iliyobebwa na jina la ‘Ukuthula,’ ikiwa na maana ya Amani.
 
Akihojiwa na gazeti la nchini mwake maana ya Ukuthula, Rebeca alisema aliamua kuipa albamu hiyo jina hilo, baada ya tafakuri ya kina juu ya mazingira halisi dunia ya sasa ilivyo ambako kuna machafuko na mifarakano kila kona.

“Watu hawana amani. Ni vita kila mahali, hata katika makanisa. Nataka watu wawe kitu kimoja kwani amani ni kitu muhimu katika maisha yao ili kudumisha amani ya dunia,” alisema Rebecca.

Mafanikio
Mafanikio makubwa ya Rebecca katika uimbaji wake yalikuja mwaka 1990, aliposhinda tuzo ya KORA iliyomfanya awe malkia wa muziki wa Injili barani Afrika.
 
Mwaka 2003, Malope alitunukiwa shahada ya Udaktari wa Falsafa kwa utumishi uliotukuka kwa umma kupitia ujumbe wa nyimbo zake zikiwa na nguvu ya kubadili mwelekeo wa maisha ya wengi.
 
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na mwakilishi wa Taasisi ya International Theological Seminary ya California, Marekani nchini Afrika Kusini, Dk. Keith C Harrington.
 
Itakuwa ni mara ya pili kwake kuja nchini kutumbuiza katika tamasha hilo kwani mara ya kwanza kuja nchini ilikuwa Aprili 6, 2012 kwa kazi ya kutumbuiza katika Tamasha la Pasaka la Aprili 8, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Waliobahatika kufika katika uzinduzi wa tamasha hilo ambalo lilianzia Uwanja wa Taifa siku hiyo kabla ya kwenda mikoani, walipata fursa ya kujionea mengi ya kuvutia kutoka kwa mwimbaji huyo na wengine.

Hicho ndicho kimewafanya wapenzi na mashabiki wengi watake mwimbaji huyo awemo katika orodha ya tamasha lijalo, hivyo kuwapa kazi ya ziada waratibu kufanikisha suala hilo kwa heshima ya mashabiki na wadau wa tamasha hilo.

2. Keke
Mbali ya Malope, safari hii kutakuwa na mwimbaji mwingine kutoka nchini humo ambaye ni Kekeletso Phoofolo  ‘Keke’ anayetamba na vibao vyake kibao vyenye mvuto wa aina yake kama ‘Sefapaanong Ke Boha.’

Keke, baba wa watoto wawili ambaye licha ya kupitia maisha ya uchokoraa, ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya, kwa sasa ni mwimbaji mahiri na kiongozi wa kanisa kama ilivyo kwa Solly Mahlangu.

Keke (32), ni kiongozi wa Kanisa la Shekinah Glory Worship Tabernacle lenye maskani yake katika mji wa Krugersdorp, likifanya vizuri huku aking’ara katika uimbaji hadi kupewa tuzo mbalimbali.

Japo kwake ni mara ya kwanza kushiriki Tamasha la Pasaka, lakini yu miongoni mwa waimbaji wenye uwezo mkubwa jukwaani, hivyo akishirikiana na wengine, tamasha la safari hii linatarajiwa kuwa na kishindo cha kipekee zaidi.

3. Faraja Ntaboba

Huyu ni mwimbaji wa kimataifa kutoka DR Congo atakayepamba tamasha hilo, akitamba na vibao mbalimbali ikiwemo albamu yake mpya iliyobebwa na jina la ‘Naomba Niseme na Wewe.’

Ntaboba aliyewahi kutikisa katika Tamasha la Pasaka la mwaka 2011 ambalo lilikuwa la mwisho kufanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, amewahi kuwika na vibao vingi moto kama ‘Yupo Mungu’  na ‘Mke wa Pili’.

Vibao vingine vya Ntaboba, ni ‘Kuku na Vifaranga’, ‘Inua Macho’, ‘Umenitoa Mbali’, ‘Mwambie Farao’, ‘Kuachwa’ na ‘Siku ya Kuinuliwa’.

Katika tamasha la Diamond ambalo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliweza kuwa Baraka, ashirikiana na wakali wengine kama Ephrael Sekereti wa Zambia, Solomon Mukubwa na Anastazia Mukabwa  kutoka Kenya.

Mukabwa akipewa sapoti na malkia wa muziki wa Injili wa Tanzania, Rose Muhando, aling’ara vilivyo kupitia kibao chake cha ‘Kiatu’ huku Boniface Mwaitege akitesa na vibao kadhaa kikiwemo cha ‘Mama ni Mama.’
4. Sara Kierie


Sara Kierie ‘Sarah K’ ni mwimbaji mahiri kutoka Kenya ambaye ametamba na vibao vingi vilivyotikisa nchini Kenya na Afrika Mashariki, kikiwemo cha ‘Liseme.’

Vibao vingine vilivyomng’arisha Sarah ni Usiyeshindwa, Mbele Ninaendelea, Mnyunyizi Wangu, Nina Sababu, Nasema Asante na vingine ambavyo vimekuwa baraka na faraja kwa wengi kutokana na ujumbe wa neno kamili la Mungu ambalo hufikishwa katika mazingira ya burudani.
 
5. Sekeleti

Ephraim Sekeleti aliyezaliwa mwaka 1983 katika mji wa Kalulushi, yu miongoni mwa waimbaji maarufu wa nyimbo za Injili nchini Zambia ambaye amethibitisha kupamba Tamasha la Pasaka.

Mwimbaji huyo aliyemaliza elimu ya sekondari mwaka 2001 katika Shule ya Kalulushi,  ni mtoto wa nne kati ya sita, aliingia katika muziki akiwa kinda akifundishwa kupiga kinanda na mmisionari akiwa na umri mdogo.

“ Ephraim alikuwa ni mtoto aliyekuwa wa kelele nyingi,” Yeye pamoja na dada zake waliimba kanisani wakitumia kinanda na huko alipata uzoefu katika uimbaji na upigaji wa kinanda,” anasema mama yake.
Baadaye alijiendeleza katika uimbaji katika kikundi cha Virtue for Christ akidumu kwa miaka miwili.

Mwaka 2002, akiwa na kiu ya kurekodi albamu yake, alijitoa mhanga kwenda Afrika  Kusini akiwa  na kiasi kidogo tu cha pesa. Akiwa huko, alirekodi nyimbo mbili tu kati ya albamu nzima.

Hata hivyo, akiwa nchini humo alibahatika kuingia katika Theater ya Pretoria na kupata fursa ya kuimba mbele ya Rais wa Afrika ya Kusini.

Nafasi nyingi ziliendelea kujitokeza zilizomsababishia kutaka kuacha kuendelea
na
muziki wa Injili ili aimbe miziki ya kidunia, lakini akaendelea kuimba Injili.
Milango ikaanza kufunguka na albamu yake ya kwanza ikawa ‘Temba Baby’ kwa maana ya Mtoto wa Miujiza.

Baada ya kurekodi, na kuuza nakala za kutosha za albamu hiyo ya ‘Temba Baby’, kwa mafanikio ya hiyo kazi Ephraim aliamua kurudi nyumbani kuwekeza ile fedha.

Alichofanya ni kuwekeza kwenye albamu  yake ya pili ya Limo Ndanaka iliyopata mafanikio makubwa.
Ni albumu iliyofanya vizuri kwenye chati mbalimbali za muziki wa Injili. Ephraim akiwa nje ya Zambia ameimba katika nchi mbalimbali zikiwemo Namibia, Afrika  Kusini, Tanzania, Zimbawe na Australia.

Sekereti amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa muziki wa Injili wa Tanzania, kutokana na ubora wa kazi zake pia upendo wa mwamuzi huyo kwa Watanzania hadi kutunga vibao kadhaa vya Kiswahili kama ‘Uniongoze,’ Baraka Zako’ na ‘Huu Mwaka’ na sasa akitesa na albamu ya ‘Vigelegele.’



6. Rose Muhando
 

Waimbaji wazawa waliothibitisha, ni malkia wa muziki wa Injili Tanzania, Rose, anayefanya kazi chini ya mkataba wa Kampuni ya Muziki ya kimataifa ya Sony Music ya nchini Afrika Kusini.

Kutokana na kushiriki kwake mara zote tamasha hili tangu mwaka 2000, ni wazi amekuwa sehemu ya tamasha hilo la kimataifa, akichangia kulipatia umaarufu tamasha hilo katika kutimiza malengo yake.

Katika mahojiano na Tanzania Daima, Rose anasema hujisikia fahari kushiriki matamasha ya Injili akitambua kuwa ni sehemu ya kurejesha shukrani kwa Mungu aliyemjaalia kipawa cha uimbaji, pia kuwashukuru wapenzi na mashabiki wake.

“Neno la Mungu ni jipya kila siku, tena ni chakula cha roho, hivyo kwa kushiriki kwangu mara zote Tamasha la Pasaka, hakuna kinachopungua, ndiyo kwanza nazidi kuimarika zaidi nikitambua nini mashabiki wangu wanataka,” anasema Rose.

Rose anawasihi wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili, wajitokeze kwa wingi katika tamasha la mwaka huu kuanzia siku ya ufunguzi Uwanja wa Taifa na pale litakapogeukia katika mikoa ambayo itateuliwa.

“Nawaomba wapendwa katika Kristo Yesu na mashabiki wa muziki  wa Injili kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Pasaka ili kusikia neno la Mungu, pia kusapoti malengo ya sehemu ya mapato kusaidia makundi ya wenye mahitaji,” anasema.

Rose ni mwimbaji aliyeng’ara na vibao vingi ambavyo ni orodha ndefu kama Jipange Sawasawa, Wololo, Nibebe, Utamu wa Yesu, Achia, Sitanyamaza, Nipe Macho, Mwanamke Mbaya, Nipe Uvumilivu, Woga Wako, Ndivyo Ulivyo, Pasipo Maono.

7. Upendo Nkone

Nyota wengine ni Upendo Nkone ambaye amekuwa baraka kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili kutokana na kushiriki kwake mara nyingi matamasha ya Msama Promotions, yaani Pasaka na Krismasi.

Mfano halisi ni katika tamasha la Krismasi la Desemba 25, 2013, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwani aliweza kuwa miongoni mwa waimbaji waliofunika siku hiyo ya uzinduzi hadi kwingineko mikoani.

Miongoni mwa vibao vilivyomng’arisha Nkone katika tasnia ya muziki wa Injili, ni Hapa Nilipo, Neno lako ni Taa, Unajibu, Unastahili Kuabudiwa, Usifurahi juu yangu, Zipo faida, Unitetee, Upendo wa Yesu, Mwambie Yesu na vinginevyo vingi. 

8. Upendo Kilahiro

Upendo Kilahiro naye yu miongoni mwa waimbaji mahiri akiwa na uzoefu mkubwa wa kushiriki matukio ya kimataifa ya muziki wa Injili ambaye amekuwa akihudumu pia nchini Afrika Kusini.

Kutokana na kipaji chake cha uimbaji, historia yake inaonesha kuna wakati Wacanada waliwahi kutamani kumpa uraia wa nchi hiyo, lakini kutokana na mapenzi yake kwa Tanzania, alisema hapana.

Aidha, Kilahiro ndiye Meneja wa mwimbaji bora wa Injili Afrika, Rebecca Malope kwa nchini Tanzania, hivyo ni bahati nyingine kwa Tanzania kuendelea kupata baraka za Mungu kupitia kwa mwanamama huyo wa Afrika Kusini.

Katika uimbaji, Kilahiro amekuwa  aking’ara na kutamba vilivyo kupitia vibao vyake vingi vyenye ujumbe na mguso wa aina yake na kuwa baraka kwa wengi, iwe katika kufundisha ama kuburudisha.

Miongoni mwa vibao vya mwanadada huyo ni ‘Hakuna Usiloliweza,’ ‘Hilo Nalo’ ‘Litapita,’‘Baba Ninakuabudu,’ ‘Zindonga,’ ‘Mungu Unaishi,’ ‘Usinipite,’‘Amen Haleluya,’ ‘Sinzogir co Ntinya,’ ‘Nani kama Wewe’ na vinginevyo.

Zikibaki wiki nne kabla ya kuziduliwa kwa tamasha hilo jijini Dar es Salaam, waimbaji waliothibitishwa wameanza kujifua kwa ajili ya tamasha hilo chini ya vyombo ya kisasa.

Msama anatoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili wa ndani na nje ya Tanzania kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Pasaka popote litakapofanyika ili kupata ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya burudani.

“Nawasihi wapendwa wote katika Kristo, wapenzi na mashabiki wa  muziki wa Injili, wajitokeze kwa wingi katika Tamasha la Pasaka, kwani kufika kwao ndio uhai wa tukio hili la kimataifa, ambapo sehemu ya mapato yatakwenda kusaidia makundi maalumu,” anasema Msama.

Anaongeza kwa kutambua umuhimu na maana ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya ufufuko wa Yesu Kristo; kwa maana ya ushindi wa mwanadamu dhidi ya dhambi, mashabiki wa muziki wa Injili walitumie kukamilisha furaha ya ushindi huo.

Msama anasema, mbali ya malengo ya kusaidia makundi maalumu katika jamii kama walemavu, wajane na yatima, pia Tamasha la Pasaka ni kielelezo cha upendo na amani kutokana na kuwavuta wengi bila kujali tofauti za dini, kabila wala itikadi za kisiasa.

Anasema tangu kuanza kwa tamasha hilo, limekuwa likiwaleta wengi pamoja bila kujali tofauti za kidini, itikadi za kisiasa wala jinsia chini ya msingi kwamba mbele
za
Mungu, kila goti litapigwa.

Msama anatoa wito kwa wadau wa muziki wa Injili kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo la kimataifa; kuanzia siku ya uzinduzi katika Uwanja wa Taifa na kwingineko katika kufanikisha malengo ya tamasha hilo.

Akifafanua, Msama anasema mbali ya tamasha hilo kuutangaza ushindi na tukufu wa Mungu, pia ni kuuinua muziki wa Injili ambao ni ajira ya uhakika kwa wenye vipaji vya uimbaji na fani nyinginezo katika tasnia hiyo.

Aidha, tamasha hilo ambalo safari hii linabebwa na kaulimbiu ya ‘Uzalendo Kwanza, Haki Huinua Taifa,’ limekuwa na malengo mengine ya msingi ambayo ni kurejesha sehemu ya mapato kwa jamii, kwa maana ya kuyapa faraja makundi maalumu kama yatima, walemavu na wajane.

 Hili ni jukumu ambalo limekuwa likifanywa na waratibu wa Tamasha la Pasaka na Krismasi, iwe kabla au baada ya tamasha husika kwa kutambua kwamba suala la kusaidia makundi hayo ni wajibu wa jamii nzima.Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment