Pages

Tuesday, June 10, 2014

AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI BAADA YA KUGONGA MARA MBILI


Mfanyabiashara wa madini, Richard Lucas (29), amejipiga risasi kichwani baada ya kusababisha ajali mbili tofauti na gari lake kupinduka.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12 jioni nyumbani kwa marehemu eneo la Kimandolu.



Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema kuwa Lucas alijipiga risasi ya kichwa kwa kutumia bastola aina ya Luger yenye namba B136986 baada ya kuwagonga watu hao.

Kamanda Sabas, alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Lucas alitokea Tengeru akiwa na gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba za usajili T 494 CKY alikokuwa amemfuata rafiki yake aliyekuwa amepata ajali ya kugongwa na gari.

Alisema kuwa walipofika eneo la Sekei Darajani, alimgonga mwendesha pikipiki na kuendelea na safari ambapo mbele kidogo aligonga daladala lenye namba za usajili T 636 CUR aina ya Nissan iliyokuwa inapakia abiria.

Kamanda Sabas, alisema baada ya hapo gari ya Lucas ilipinduka na waliokolewa kwa kupitia dirishani na wananchi, ndipo marehemu aliondoka eneo la tukio kwa pikipiki ya kukodi akielekea nyumbani kwao Kimandolu huku akimuacha Vick Mchuma kwenye eneo la tukio.

Alisema kuwa baada ya muda, Mchuma ambaye waliongozana naye kwenda kumsaidia rafiki yao aliyepata ajali Tengeru, alipata taarifa kuwa Lucas amejipiga risasi.

Katika tukio jingine, mpanda milima, Denis Joel, ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali chini ya bega la kulia karibu na moyo alipotofautiana na mtu aliyekuwa akimdai shilingi 40,000.

Kamanda Sabas, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili asubuhi kwenye Kitongoji cha Olturei-Moivo wilayani Arumeru.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Joel alichomwa na kitu hicho na mtuhumiwa, Solomon Lembris, ambaye walitofautiana kauli wakati wakidaiana fedha.

“Baada ya kuona jeraha, Joel aliamua kukimbia na Lembris aliendelea kumkimbiza kuhitaji amlipe pesa zake ambapo aliishiwa nguvu na kuanguka chini kisha kupoteza fahamu na kufariki dunia,” alisema Kamanda Sabas.

Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo, Lembris alitokomea kusikojulikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Tukio jingine ni la mkazi wa Sokon II, Arumeru, Lalaito Ngitoo (50), aliyekutwa amekufa na mwili wake ukiwa kwenye maji ndani ya Mto Kijenge bila jeraha.

Kamanda Sabas alisema tukio la kifo cha Ngitoo, lilitokea juzi majira ya saa 11 ambapo kabla ya mwili wake kukutwa Mto Kijenge, alitoweka nyumbani tangu Juni 7, mwaka huu.

Alisema kuwa Ngitoo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa ambao humsababisha kuanguka mara kwa mara.
Kamanda Sabas alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru.TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment